Jumatano, 12 Oktoba 2016

Faida za kutumia rasilimali ya gesi asilia kama chanzo cha nishati ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati.

Habari ya mizunguko ya hapa na pale Mtanzania mwenzangu? Ni siku nyingine tena Mwenyezi Mungu ametupa uhai wa bure basi na tuufanyie kazi ipasavyo.


Leo tunaangalia faida za gesi asilia mpaka sasa katika jamii yetu ya Kitanzania hasa kwanza kwa jamii ambayo gesi hii imegunduliwa halafu tutaangalia faida kwa Taifa kwa ujumla.


Pia nikukumbushe tu kwamba ili Taifa lifaidike kihalali katika ugunduzi huu wa gesi asilia ni wazi kwamba kunatakiwa kuwepo na usimamizi dhabiti, sheria na mikataba ambayo itainufaisha nchi. Kinyume na hapo tutakuwa watazamaji tu wa rasilimali hii muhimu duniani na tutaishia kuwafaidisha wenzetu wa nje. Viongozi wetu (wa serikali) wana dhamana kubwa sana katika kuhakikisha hili linafanikiwa.


Faida ya rasilimali hii kiujumla (gesi asilia) kama chanzo cha nishati ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati:

o   Kiuchumi si ghali kama zingine zipatikanazo chini ya ardhi kama mafuta na madini mengine ambayo yaliyopo na hata vifaa vinavyotumia gesi asilia havina gharama kubwa kama vile vinayotumia umeme au nishati nyingine zilizopo tayari. Mfano mzuri ni majiko ya gesi, pasi za gesi na heater za gesi.
o   Kimazingira ni rafiki wa mazingira kwanza kwa sababu haichafui ardhi maana mabaki yake yapo katika hali ya hewa. Hivyo hayagusi ardhi wala vyanzo vyetu vya maji tofauti na vyanzo vingine vya nishati ambavyo vikitumiwa huleta madhara makubwa katika hewa, ardhi na vyanzo vya maji. Ukitaka kunielewa angalia uchafuzi unaofanywa na vyanzo vya nishati za kumiminika kama mafuta ukilinganisha na huu wa gesi.
o   Kiusafirishaji rasilimali hii husafirishwa kupitia baharini na ardhini jambo linalorahisisha usafirishaji wake ukilinganisha na rasilimali nyingine ambazo pia hutumia bahari kwa baadhi ya maeneo lakini kwa asilimia kubwa zinazotegemea barabara na treni kama njia za usafirishaji.
o   Pia rasilimali hii ina matumizi mbali mbali kwa viwango tofauti. Rasilimali hii ni chanzo cha nishati ya kuendesha mitambo mbali mbali ya uzalishali mali kama umeme, magari na uzalishaji wa mbolea, plastic na vitu vingine vingi.
o   Upatikanaji wake hasa kwa nchi yetu ni mkubwa kama ilivyoelezwa katika chapicho iliyopita 57 trillion feet cubic.



Sasa tuangalie faida za gesi kwa jamii yetu ya Kitanzania tangu ugunduzi wake kwenye maeneo yalipotokea ugunduzi huo kama Wizara ya Nishati na madini inavyo eleza katika ripoti yake ifuatayo:


Huduma za Jamii

o   Katika mikoa ya Lindi na Mtwara kumejengwa shule za upili pamoja na kuzikarabati (mabweni) zile ambazo tayari zimeshajengwa hapo awali.
o   Uboreshwaji wa zahanati ya Songo songo na kuongezwa vifaa muhimu Zaidi.
o   Ajira za moja kwa moja kwa wananchi wa eneo husika Lindi na Mtwara.
o   Kila mwaka wanafunzi kumi bora waliofaulu wanafadhiliwa na mradi kwenda shule ya Sekondari ya Makongo. Wanafunzi hawa wanaofaulu vizuri watafadhiliwa hadi vyuo vikuu;
o   Kodi ya huduma inayolipwa kwa Halmashauri za Lindi na Mtwara inayosaidia katika maendeleo ya Halmashauri husika.
o   Miradi ya maji pamoja na barabara pia imefanyika kwa ajili ya wananchi.



Kwa taarifa kamili kuhusiana na rasilimali hii ya gesi nitakuwekea ripoti kutoka Wizara ya nishati na madini muda si mrefu upate kujua zaidi kuhusiana na faida zake kwa wananchi wa Mtwara na Lindi mpaka sasa.

Nikutakie siku njema na yenye baraka. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni