Jumamosi, 12 Novemba 2016

Jifunze na jihabarishe kuhusiana na magari yanayoyumia gesi na mafuta "bi-fuel".

Mpenzi msomaji u hali gani?
Leo napenda nikufahamishe kuhusiana na uwepo wa magari tajwa hapo juu. Ni magari yenye uwezo wa kutumia mfumo mmoja baada ya mwingine. Inamaana kuna mfumo wa gesi na mfumo wa mafuta ya dizeli ama petroli. Hivyo basi unaweza kujaza gesi na inapokwisha mfumo wa mafuta uka "pick" na kuendelea kuendesha gari bila ugumu wowote. Angalia picha zifuatazo zinazoonesha bi-fuel system.























Magari yanapotumia gesi inaweza kuwa "liquefied natural gas" (gesi ilihifadhiwa katika hali ya kimiminika) au "compressed natural gas" gesi asilia iliyo katika hali ya hewa. LNG "liquefied natural gas" inatoa nishati ya kuendesha gari sawa sawa na nishati inayoweza kutolewa na petroli. LNG inahitaji asilimia 30 tu ya nafasi katika tanki la CNG (compressed natural gas) ili kuhifadhi gesi kimiminika inayoweza kuzalisha nishati ya kuendeshea gari kama ile ya CNG. Kwa maana hiyo LNG inatumika kidogo kulinganisha na CNG kuzalisha nishati kubwa kuendesha gari. Ili  LNG iwe ya baridi inahifadhiwa katika matanki yaliyo nje ya gari, Injini inapowashwa gesi inapashwa moto na kuwa katika hali ya kimiminika tena na kuanzia hapo mfumo unafanya kazi kama ule wa CNG.

Kumbuka:
Kituo chetu cha Songosongo kinajaza gesi aina ya CNG. 



Ahsante kwa usomaji wako na alamsiki. 
Kwa maoni, ushauri na maswali tuandikie katika sanduku la maoni au kupitia:
1. 0765749191
2. kitahsiyame@gmail.com





Jumatatu, 7 Novemba 2016

Je, unafahamu ni vitu gani vingine vinavyotumia gesi kuzalisha nishati na kujiendesha mbali na majiko ya gesi?

Vipo vingi,
1. Magari
2. Pasi za kunyoshea
3. Mashine za kuzalisha umeme
4. Mashine za kufulia na mashine za maji (kwa nchi zilizoendelea)
5. Na mifumo ya kupasha joto nyumba (kwa nchi zilizoendelea pia)


Tuzungumzie gesi katika magari. Kuna magari hutumia gesi tu kama “fuel” na mafuta tu kama “fuel” na yale yanayotumia vyote (bi-fuel) mafuta na gesi kama “fuel”. Yale yanayotumia gesi huwa na muonekano kama huu kwa ndani. Gesi inayotumiwa na magari inaweza kuwa katika hali moja kati ya hizi, "Gesi asilia iliyokandamizwa" kwa Kiingereza "compressed natural gas" au "gesi asilia katika hali ya kimiminika" kwa Kiingereza "liquified natural gas". Kwa hapa kwetu Tanzania kituo chetu cha songo songo kina toa "Compressed Natural Gas". Na mitungi ya gesi huwa katika nafasi tofauti kama utakavyoona katika picha hapa chini. 





Na hapa chini ni mfano wa sheli zinazo jaza gesi magari kama "fuel" kwa nchi za wenzetu zilizoendelea, ambapo idadi ya vituo vya kujazia ni kubwa kwao japokuwa wengine si wazalishaji wakubwa kama sisi tulivyo wazalishaji wakubwa na kituo tulichonacho ni kimoja tu cha Songo songo pale Ubungo karibu na kiwanda cha Chibuku na ofisi za twiga cement. 


                                





Na hiki ni kituo chetu cha kujazia gesi kwenye magari hapa nchini kwetu.











Mpenzi msomaji wataalamu wa masuala ya nishati duniani wameainisha kwamba gesi kama fuel ni nzuri zaidi kimatumizi kuliko mafuta (petroli na dizeli). Sababu kuu ni kwamba gesi asilia ni rafiki wa maziningira na pia kiutumikaji gesi inatumika kidogo na kuzalisha nguvu kubwa wakati kulinganisha na mafuta. Hivyo basi kwa wale wenye uwezo tayari wameanza kutumia magari yanayo tumia gesi na wengine wanatumia magari yenye uwezo wa kutumia gesi na mafuta kwa pamoja ambapo kunakuwa na auto shift ya system. Kwamba mafuta yakiisha basi mfumo wa gesi unaanza kuendesha gari. Haya ni machache bado na kwa Tanzania sina uhakika kama yamefika japo kuna tetesi watu wanayo pia. Mfumo wake unakuwa kama huu pichani. 


Picha kwa hisani ya http://www.picautos.com/


Je, pamoja na sisi kuwa wazalishaji wa gesi kuna manufaa ya kuwa na gari inayotumia gesi nchini?

Kwanza kabisa utambue kituo cha kujazia gesi ni kimoja pale Ubungo, kama mizunguko yako ni ya karibu na pale hakuna tatizo utafaidika. Kama mizunguko yako inafika mbali hautafaidika kabisa maana ukiishiwa gesi hutakuwa na pa kujazia utakwama njiani. Serikali yetu inatakiwa ilitazame suala ili kwa upya. Gesi ina manufaa makubwa sana kama itakuwa makini kusimamia rasilimali hii kwa ufanisi kwa sababu kwanza kabisa inachimbwa ndani ya nchi yetu. 

Hivi sasa kuna mipango ya kujenga mabomba ya kusafirisha nchi jirani, na kabla ya kuisafirisha kwa nchi jirani inatakiwa sisi Watanzania tufaidike KWANZA. Mambo ya "business as usual" yawekwe pembeni. Mikataba na taratibu zote za uwekezaji itufaidishe sisi wananchi kwanza. Imekuwa suala la kawaida kwa nchi za Africa kuwa na rasilimali ADIMU na bado kuwa nchi masikini. Viongozi wetu mna dhamana kubwa sana katika hili na tukumbuke mabadiliko yanaletwa na sisi wenyewe wenye nchi, hakuna mzungu wala malaika atakae kuja kutubadilishia uchumi wetu. 


Kwa habari zaidi kuhusiana na matumizi ya gesi katika gari usikose kusoma post inayofuata.


Kwa maoni, ushauri na maswali tafadhali tuandikie katika boksi la maoni hapo chini au kupitia
1. 0765749191
2. kitahsiyame@gmail.com

Jumanne, 25 Oktoba 2016

Jifahamishe ni jinsi gani gesi asilia huchimbwa.

Mpenzi msomaji habari yako?
Leo tutajifunza namna ambavyo rasilimali hii ya gesi asilia inavyochimbwa. Kwanza kabisa kijiografia gesi asilia inapakana na leya ya mafuta kwa chini na "shale" kwa juu ikifuatiwa na makaa ya mawe na miamba mengine juu yake zaidi.






Gesi ni matokeo ya mkandamizo na uozo wa viumbe hai (wanyama na mimea) iliyokufa miaka zaidi ya milioni iliyopita. Gesi asilia kikemikali ni methane CH4 lakini ndani yake kuna kemikali nyingine kama propane, ethane na hydrocarbon kubwa nyingine. Pia ina nitrogen kwa kiasi kidogo, kabonidayoksaidi, hydrogen sulphide na maji pia.

Mashine kubwa na za kisasa huingizwa ndani ya ardhi mpaka kule ambako rasilimali hii inapatikana ambapo inakuwa imechanganyikana na rasilimali nyinginezo. Sasa basi baada ya gesi kuchimbwa hupitishwa katika mitambo mingine ambayo huikausha na kuitengeneza tayari kwa ajili ya kuisafirisha katika mabomba (pipelines) kutoka machimboni kwenda maeneo yenye uhitaji kama Dar es Salaam.

Iwapo itasafirishwa kama ilivyo inaweza kuleta madhara kwa mabomba hayo ndio maana lazima iwe "treated" ili ifike salama. Na pia katika njia ya usafirishaji huwa kuna kuwepo na vituo mbali mbali ambavyo kazi yake ni kuongezea pressure kwa gesi inayosafiri ili mwendo wake usipungue njiani na kukwama. Vituo vyote hivi huwa vinasimamiwa na kompyuta na hata watu pia wakati mwingine kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa vituo hivyo pamoja na gesi inayosafiri.















Mpenzi msomaji, kitaalamu gesi asilia huwa haina harufu, lakini makampuni yanayochimba na kutengeneza gesi kwa ajili ya matumizi mbalimbali kwa watu huchanganya gesi hiyo na kemikali nyingine ambayo inaifanya iwe na harufu kama ya yai lililooza ili kusaidia kufanya utambuzi pale inapotokea ikavuja kuzuia maafa makubwa.

Kwa makala kama hizi usiache kufungua ukurasa wako kupitia kiungo hiki uhabarike zaidi https://oilinagesi.blogspot.com




Kwa maoni na ushauri usisahau kutuandikia kupitia sanduku la maoni hapo chini au kupitia
1. 0765749191
2. kitahsiyame@gmail.com

Ijumaa, 21 Oktoba 2016

Je, unaijua harufu ya gesi ya jiko kama ikitokea inavuja?

Habari ya leo mpenzi msomaji wangu. Ni matumaini yangu u mzima.
Ni vizuri unapotumia jiko la gesi ujue harufu ya gesi ili kama inakasoro ya kuvuja uwahi kuinusuru. 
Gesi ya kupikia hunuka kama yai lililooza. Mara unaponusa harufu hii chukua hatua za ziada kama tulivyoona katika chapisho lililopita. 

Kumbuka:
1. Kumbuka gesi inatakiwa ikae chini kwa usalama na jiko liwe juu au mtungi ukae nje.
2. Ikitokea gesi ikavuja zima jiko kwenye koki pia fungua madirisha na milango ili hewa isafishike         na kisha toa jiko nje kwa ukaguzi kama unaweza ama toa taarifa kwa watu uwajuao.
3. Nunua gesi na jiko kwa mtu anaetambulika na serikali kufanya biashara hiyo na sio matapeli               kuepuka maafa.


Kwa maoni na maswali tuandikie kupitia sanduku la maoni hapo chini au
1. 0765749191
2. kitahsiyame@gmail.com

Jumanne, 18 Oktoba 2016

Gesi ya jiko inapovuja unatakiwa ufanye haya haraka sana.

Mpenzi msomaji, habari ya mihangaiko ya hapa na pale.

Leo tuna angalia mambo ya kufanya pale unaponusa gesi ya jiko ndani ya nyumba. Sote tunajua kwamba gesi asilia inayotumika kupikia majumbani ina harufu fulani ambayo ni tofauti na hewa nzuri tunayovuta. Hewa safi anayovuta binadamu haina harufu, lakini gesi asilia ina harufu. Kama umetumia mara kadhaa jiko la gesi utakuwa unaelewa nini nazungumzia.


Gesi asilia ni sumu?

Kama tulivyoona katika chapisho lililopita kwamba ikivutwa kwa kiasi kidogo si mbaya. Iwapo itavutwa kwa kiasi kikubwa ndio huleta madhara. (tizama chapisho linalohusu hasara za kutumia gesi asilia). Ila kwa kukusaidia wewe ambae hukupata nafasi kuisoma post hiyo ni kwamba unapovuta gesi asilia ina maana utakosa oksijeni inayoweza kupelekea kujisikia kizungunguzungu, mamumivu ya kichwa, uchovu na hata kuzimia na kifo kwa baada ya muda mrefu. 

Haya ni ya kufuata unapohisi au nusa gesi inayovuja katika jiko la gesi ndani ya jengo ulilopo:

1. Zima jiko la gesi kama unajua kuzima na kwenye mtungi pia kama unaweza kuzima pia. 
2. Usivute sigara, usiwashe moto wa aina yoyote kwa kiberiti au namna yoyote, usiwashe na kuzima swichi za umeme, usitumie simu ya mkononi wala ya mezani. 
3. Fungua milango, madirisha na ondoka ndani ya jengo hilo haraka.
4. Kisha piga simu kwa aliekuuzia gesi kama ni mtu au kampuni hasa kituo ulichochukulia mtungi au fundi aliekufungia mtungi huo wa gesi. Kama hayo yote yatashindikana unaweza wasiliana na watu wa fire wakakupa maelekezo ya kufanya. 


Jumatatu, 17 Oktoba 2016

Dondoo muhimu za kukuhakikishia usalama wako unapotumia jiko la gesi au vifaa vingine vinavyotumia gesi.

Mpenzi msomaji habari ya jumatatu?

Leo tutaangalia dondoo kadhaa muhimu kwa ajili ya usalama wetu tunapotumia vifaa vya gesi hasa majiko ya gesi ambayo tunatumia kwa sehemu kubwa katika jamii yetu.

1. Hakikisha unanunua gesi kwa muuzaji mwenye kibali cha kufanya biashara hiyo (atambulike na serikali).

2. Kama ni jiko linalohitaji ufungaji wa mtungi wa gesi kama huu hapa chini, tafadhali hakikisha unapata fundi mwenye utaalamu na ujihakikishie hilo, usichukue kishoka. 

Najitolea mfano mimi mwenyewe, nilimwita fundi aje kunifungia mtungi wa gesi nje, Kumbe alivyofunga hakufunga vizuri ikawa inavuja na kwa sababu ni mara ya kwanza kutumia hatukujua kama gesi inavuja kwa sababu eneo jiko lilipo ni wazi hivyo gesi ikitoka inachanganyikana na hewa hivyo hatukuweza kuihisi. Tulipotaka kulitumia siku iliyofuata, tukaliwasha na hapo hapo likalipuka bahati nzuri tukawahi kuuzima moto kwa kuzima kwanza mtungi na ule na kuutoa nje. Hivyo umakini ni muhimu sana.

3. Pia hakikisha rangi ya moto inayowaka ni bluu kama tulivyoonesha kwenye chapisho  iliyopita.



4. Jiwekee utaratibu wa jiko la gesi kukaguliwa hata mara moja kwa mwaka kuangalia usalama wako ili kama kunakifaa kinaubovu ubadilishe mapema kukwepa maafa yoyote hasa yatokanayo. Vifaa kama koki na mipira ni muhimu sana.

5. Pia zijue dalili za kulewa gesi asilia kama ikitokea ilikuwa inavuja na hukuweza kuitambua. Ambazo ni ukosefu wa oksijeni mwilini unaoweza kupelekea kutokea kwa kizunguzungu, uchovu, kichefuchefu na uhemaji usio mzuri kiafya.

6. Unapomaliza kutumia jiko la gesi hasa wakati wa usiku ni salama zaidi kama utalizima na kwenye mtungu wake.

Kwa maoni wasiliana nasi kupitia sanduku la maoni hapo chini au kupitia
1. Barua pepe: kitahsiyame@gmail.com
2. Simu no:      0765749191


Ahsante sana kwa usomaji wako washirikishe na wengine ili tuwe na jamii salama. 





Ijumaa, 14 Oktoba 2016

Je unaujua rangi ya moto sahihi unaotakiwa kuwaka unapotumia jiko la gesi?

Mpenzi msomaji Watanzani wengi sasa wameanza kuwa watumiaji wakubwa wa majiko ya gesi na hii ni kutokana na urahisi wa kutumia teknolojia hii na utendaji wake wa haraka katika kupika. Leo nitakuonesha picha zinazoonesha rangi ya moto sahihi inayotakiwa kuwaka unapotumia jiko la gesi.


Moto Sahihi –ambao rangi yake inatakiwa iwe ni bluu kama unavyoona pichani.



Moto usio Sahihi-ambao una rangi ya njano.



Linganisha vizuri uone tofauti mmoja ni bluu (sahihi) mwingine ni njano (si sahihi).



Ufanye nini sasa unapoona moto wa jiko lako sio Sahihi?


1.       Kwanza weka sawa koki au switch inayofungulia gesi kwa jiko kama hili chini pichani.

2.       Ikishindikana onana na fundi mtaalamu wa majiko ya gesi usichukue mtu limradi tu amekwambia ni fundi jiridhishe. Kuna watu hujifanya mafundi lakini hamna wanachojua matokeo yake majiko huleta maafa baadae kwa sababu tu ya uchu wao wa fedha.
3.   Washirikishe na wenzako ili jamii yetu iwe salama. Kumbuka kinyume na hapo ni kuhatarisha maisha yetu sote.

Ahsanteni na usisahau kutuachia maoni yako katika sanduku letu la maoni.

Jumatano, 12 Oktoba 2016

Je, wajua maafa ya nayoweza sababishwa na matumizi ya gesi asilia katika mazingira yako na afya yako kwa ujumla?

Mpenzi msomaji wa bloggu yetu leo tutaangalia madhara ya kutumia rasilimali hii katika mazingira yetu na kwetu sisi wenyewe.




o   Kwa mwili wa binadamu ni sumu iwapo itavutwa (na kuingia katika mfumo wa upumuaji wa binadamu). Ikivutwa kwa kiwango kidogo haina tatizo. Ila ikivutwa kwa kiasi kikubwa kwa muda mrefu itasababisha upungufu wa oksijeni mwilini hali inayoweza kupelekea kutokea kwa kizunguzungu, uchovu, kichefuchefu na uhemaji usio mzuri kiafya.

Angalizo: Uwe makini unapotumia vifaa vinavyotumia gesi asilia hasa majiko ya kupikia. Hakikisha unapolitumia/usipolitumia hakuna uvujaji wa gesi kuepusha maafa.

o   Rasilimali hii ni rasilimali isiyokuwa na mbadala mara inapovunwa au kwa kiingereza tuna sema ni “nonrenewable” energy source. Inapotumika haiwezi kufanywa tena kwa matumizi mengine, hivyo basi tujue rasilimali hii inapochimbwa kiwango chake kinazidi kupungua.

o   Ni rasilimali ambayo usafirishaji wake unagharama na una hitaji teknolojia ya juu kwa sababu mara nyingi ni lazima isafirishwe katika mabomba (pipeline) na kuwekea kemikali fulani za kusaidia usafirishaji salama.


o   Pia gesi asilia ina uwezo wa kulipuka/kuwaka na kusababisha maafa kama kuunguza nyumba na samani na hata pia mwili wa mtu.


o   Katika kuitengeneza na kuitakasa rasilimali hii inapovunwa, kuna gesi ambazo pia hupatikana kama mabaki ambazo si nzuri kwa afya ya binadamu zisipodhibitiwa vizuri.


Haya ni baadhi ya maafa mpaka sasa kutokana na kiwango chetu cha matumizi ya gesi. Maafa yanaongezeka kutokana na kiwango cha matumizi na jinsi mfumo wa usafirishaji gesi kwenye makazi ya watu ulivyojengwa ambapo kwa Tanzania sasa bado hatujafikia kiwango hicho. Nchi zilizoendelea wana mifumo ya kupitisha gesi kwenye makazi kama moja ya huduma za kijamii kama vile maji na umeme. Ni mipango ya serikali hapo mbeleni kuwa suala hili litaingia katika mpango mkakati wa kuutekeleza kama moja ya huduma ya kijamii kwa kila kaya japokuwa  ni wa gharama kubwa sana.


Kwa maoni, ushauri na maboresho tafadhali wasiliana nasi kupitia sanduku la maoni hapo chini au 
         1. kitahsiyame@gmail.com au 
         2. kwa namba 0765749191

Ahsanteni na alamsiki.

Faida za kutumia rasilimali ya gesi asilia kama chanzo cha nishati ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati.

Habari ya mizunguko ya hapa na pale Mtanzania mwenzangu? Ni siku nyingine tena Mwenyezi Mungu ametupa uhai wa bure basi na tuufanyie kazi ipasavyo.


Leo tunaangalia faida za gesi asilia mpaka sasa katika jamii yetu ya Kitanzania hasa kwanza kwa jamii ambayo gesi hii imegunduliwa halafu tutaangalia faida kwa Taifa kwa ujumla.


Pia nikukumbushe tu kwamba ili Taifa lifaidike kihalali katika ugunduzi huu wa gesi asilia ni wazi kwamba kunatakiwa kuwepo na usimamizi dhabiti, sheria na mikataba ambayo itainufaisha nchi. Kinyume na hapo tutakuwa watazamaji tu wa rasilimali hii muhimu duniani na tutaishia kuwafaidisha wenzetu wa nje. Viongozi wetu (wa serikali) wana dhamana kubwa sana katika kuhakikisha hili linafanikiwa.


Faida ya rasilimali hii kiujumla (gesi asilia) kama chanzo cha nishati ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati:

o   Kiuchumi si ghali kama zingine zipatikanazo chini ya ardhi kama mafuta na madini mengine ambayo yaliyopo na hata vifaa vinavyotumia gesi asilia havina gharama kubwa kama vile vinayotumia umeme au nishati nyingine zilizopo tayari. Mfano mzuri ni majiko ya gesi, pasi za gesi na heater za gesi.
o   Kimazingira ni rafiki wa mazingira kwanza kwa sababu haichafui ardhi maana mabaki yake yapo katika hali ya hewa. Hivyo hayagusi ardhi wala vyanzo vyetu vya maji tofauti na vyanzo vingine vya nishati ambavyo vikitumiwa huleta madhara makubwa katika hewa, ardhi na vyanzo vya maji. Ukitaka kunielewa angalia uchafuzi unaofanywa na vyanzo vya nishati za kumiminika kama mafuta ukilinganisha na huu wa gesi.
o   Kiusafirishaji rasilimali hii husafirishwa kupitia baharini na ardhini jambo linalorahisisha usafirishaji wake ukilinganisha na rasilimali nyingine ambazo pia hutumia bahari kwa baadhi ya maeneo lakini kwa asilimia kubwa zinazotegemea barabara na treni kama njia za usafirishaji.
o   Pia rasilimali hii ina matumizi mbali mbali kwa viwango tofauti. Rasilimali hii ni chanzo cha nishati ya kuendesha mitambo mbali mbali ya uzalishali mali kama umeme, magari na uzalishaji wa mbolea, plastic na vitu vingine vingi.
o   Upatikanaji wake hasa kwa nchi yetu ni mkubwa kama ilivyoelezwa katika chapicho iliyopita 57 trillion feet cubic.



Sasa tuangalie faida za gesi kwa jamii yetu ya Kitanzania tangu ugunduzi wake kwenye maeneo yalipotokea ugunduzi huo kama Wizara ya Nishati na madini inavyo eleza katika ripoti yake ifuatayo:


Huduma za Jamii

o   Katika mikoa ya Lindi na Mtwara kumejengwa shule za upili pamoja na kuzikarabati (mabweni) zile ambazo tayari zimeshajengwa hapo awali.
o   Uboreshwaji wa zahanati ya Songo songo na kuongezwa vifaa muhimu Zaidi.
o   Ajira za moja kwa moja kwa wananchi wa eneo husika Lindi na Mtwara.
o   Kila mwaka wanafunzi kumi bora waliofaulu wanafadhiliwa na mradi kwenda shule ya Sekondari ya Makongo. Wanafunzi hawa wanaofaulu vizuri watafadhiliwa hadi vyuo vikuu;
o   Kodi ya huduma inayolipwa kwa Halmashauri za Lindi na Mtwara inayosaidia katika maendeleo ya Halmashauri husika.
o   Miradi ya maji pamoja na barabara pia imefanyika kwa ajili ya wananchi.



Kwa taarifa kamili kuhusiana na rasilimali hii ya gesi nitakuwekea ripoti kutoka Wizara ya nishati na madini muda si mrefu upate kujua zaidi kuhusiana na faida zake kwa wananchi wa Mtwara na Lindi mpaka sasa.

Nikutakie siku njema na yenye baraka. 

Jumanne, 11 Oktoba 2016

Je, unafahamu nini kuhusu nishati ya gesi asilia nchini kwetu Tanzania na duniani kwa ujumla?

Tunapozungumzia nishati ya gesi, tunazungumzia nishati ambayo kwa asilimia kubwa sasa imeanza kufahamika kwa Watanzania wengi. Ni nishati ambayo hutumika katika kuendesha mitambo mbali mbali ya uzalishaji kama mitambo ya umeme, kuendesha magari na kwa matumizi ya nyumbani hasa katika majiko ya oven na ya kawaida, kuchemshia maji, kutengeneza joto, mashine za kukaushia nguo na vifaa vingine mbali mbali. 
Kwa Tanzania habari za gesi asilia zilianza kusikika miaka ya 1952 ambapo uchunguzi wake kulianza kufanyika. Mnamo mwaka 1974 kulitokea ugunduzi wa nishati hii ya gesi katika eneo liitwalo Songo Songo wilayani Kilwa katika mkoa wa Lindi. Baadae tena mwaka 1982 ugunduzi wa pili ulifanyika mkoani Mtwara (mkoa unaopakana na Lindi) eneo linaloitwa Mnazi Bay. Mpaka mwaka huu 2016 February Waziri wa Nishati na madini alieleza kuwa tani 2.7 trillion cubic za gesi asilia ziligunduliwa tena eneo la  Bonde la Mto Ruvu na kufanya jumla ya 57 trillion cubic feet ya hazina ya gesi iliyoko katika ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki. Uchunguzi wa nishati ya gesi ulifanywa na makampuni mbalimbali ya Kimataifa yenye ujuzi kuhusu nishati hii ya gesi kutoka Asia na Ulaya kama BG Group na United Arab Emirate's Dodsal Group na mengineyo ambapo baadhi yao tayari wameshajikita katika uvunaji wa gesi hii asilia kwa ajili ya matumizi mbalimbali hapa Tanzania. Upatikanaji wa nishati ya gesi asilia nchini kwetu unaweza kuwa chachu kubwa ya maendeleo nchini ikiwemo kupunguza umasikini na kuboresha huduma mbali mbali za jamii.

Je, ugunduzi huu wa gesi asilia una umuhimu gani katika uchumi wa nchi yetu?



Tukutane kesho tujuzane zaidi....